Enrolment options
Moduli hii yenye anwani ya "Uhakiki wa Kifasihi, Elimumitindo na Uandishi wa Bunilizi" ina sehemu kuu mbili. Sehemu ya kwanza inahusiana na nadharia za uhakiki wa fasihi na sehemu ya pili inahusiana na uandishi wa bunilizi.
Katika sehemu ya kwanza, moduli hii inajikita katika kutalii maana ya nadharia, sifa za nadharia, maana ya nadharia za uhakiki na tofauti yake na nadharia ya fasihi na uhakiki. Dhana muhimu kama vile mhakiki na uhakiki zinashughulikiwa pia. Aidha, nadharia za uhakiki zinagawanywa kwa namna zinavyohusiana katika makundi makuu manne. Kila nadharia iliyopo kwa kila kundi inafafanuliwa huku mihimili yake ikiwekwa bayana. Mkaza unawekwa katika kumfundisha mwanafunzi namna ya kuzitumia nadharia katika kufanya uhakiki. Katika sehemu hii ya kwanza, pia kuna mada nyingine zinzohusiana na fasihi ya watoto na fasihi linganishi.
Sehemu ya pili inamakinika zaidi na ujifunzaji wa utunzi wa kazi za kubuni au bunilizi kama taaluma. Hivyo, inaoneshwa ni kwa namna gani mtu anaweza kujifunza bunilizi na kuepuka mtazamo potofu kuwa watunzi wa bunilizi ni wale tu waliozaliwa wakiwa na vipaji. Katika sehemu hii, suala pia la uandishi mzuri linapewa kipaumbele. Hii inafanyika kwa kuweka mkazo katika mambo mawili: uandishi sahihi na uzingatiaji wa wa kiwango cha juu cha usanifu.
Kwa hakika, moduli hii inaweka mkazo zaidi katika nadharia na vitendo. Maarifa pasipo kujua namna ya kuyatumia hayana maana yeyote katika dunia ya sasa.